RIDHIWANI AFUNGUKA TENA TUHUMA DAWAZA KULVYA
Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, amezungumzia suala la marafiki zake kuhusishwa na biashara ya dawa za kulevya huku akisisitiza kwamba wanaodaiwa kuwa ni marafiki zake sio bali ni watu anaokutana nao katika maeneo anayotembelea.
Mbunge huyo amezungumza hayo jana jijini Dar es Salaam baada ya kuhojiwa na Mamlaka ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya nchini, ambapo alisema roho yake imesuuzika kwani jamii imeamini kwamba hahusiki kwa namna yoyote ile na biashara hiyo haramu.
Ridhiwani alieleza kufurahishwa kwake baada ya kuhojiwa na Mamlaka hiyo nchini.
“Nashukuru kwa kuhojiwa huku nimepata nafasi ya kueleza ukweli juu ya jambo hili ambalo lilishaanza kuleta taharuki katika jamii, sasa umma umejua kuwa siuzi wala sihusiki na dawa za kulevya, roho yangu imesuuzika,” alisema Ridhiwani.
Alisema vita ya dawa ya kulevya ni kubwa na inapaswa kupigwa na kila mmoja ili kuokoa kundi kubwa la vijana ambao wanaathirika kutokana na suala hilo na kwamba kuhojiwa kwake kumemfanya awe na amani.
“Naunga mkono vita hii ya dawa za kulevya nchini kwani itasaidia kurudisha nguvu kazi inayopotea kutokana na matumizi ya dawa hizo za kulevya kwa mzazi ambaye mtoto wake ameathirika na matumizi ya dawa hizo anajua uchungu wake na hasara zake,” alisema Ridhiwani.
Aidha, aliongeza kuwa jamii inapaswa kusimama kwa kauli moja ili kuliokoa Taifa na nguvu kazi inayopotea ili Taifa liwe na vijana wanaojitambua na kutimiza wajibu wao katika kulitumikia taifa.
Ridhiwani alisema mchakato huo wa kupambana na dawa za kulenya nchini umekuwa ukiwachanganya wananchi kwani haieleweki ni nani anayehusika na kushugulikia suala hilo.
“Huu mchakato umekua ukichanganya, kuna watu wanaitwa kwa Kamanda Sirro na wengine wanaitwa kwa Kamishna Sianga (Rogers), mfano msanii Vanessa Mdee ambaye ameitwa kwa Kamanda Sirro badala ya kwa Kamishna Sianga,”alisema Ridhiwani.
Alisema watu wanahoji kwanini wengine watangazwe hadharani na wengine kuitwa kimya kimya na ameongeza kuwa ni vyema mamlaka zikajipanga ili kufanikisha vita hii na kufikia malengo yake ya kumaliza tatizo la dawa za kulevya nchini
Post a Comment