Header Ads

SOMA!! RAIS MAGUFULI ANAVYOZIMA KIKI ZA MAWAZIRI....!!!



KAMA kuna waziri au kiongozi yeyote anataka kutoa taarifa yenye kuwagusa wananchi moja kwa moja, ni dhahiri kuwa sasa atalazimika kujiridhisha zaidi.

Aidha, waziri na viongozi wengine wanatakiwa pia kuzingatia dhana ya uongozi wa pamoja kwa kuwahusisha wenzao na pia kupata maoni ya wataalamu katika wizara au taasisi wanazoziongoza kabla ya kulifikisha kwa umma.

Vinginevyo, mawaziri wajiandae kushuhudia maagizo yao yakitenguliwa huku pia wakijiweka katika hatari ya kufikiriwa kuwa wanafanya hivyo kwa minajili ya kutumia matamko yao kama ‘kiki’ za kuwaonyesha kuwa wanafanya kazi vyema na kwa kasi inayosisitizwa na Serikali ya awamu ya tano.

Angalizo hilo limetolewa na baadhi ya wachambuzi wa amsuala ya kisiasa walizoungumza na Nipashe kuelezea mkasa uliomkuta Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye agizo lake la kuzuia ufungishaji ndoa kwa watu wote wasiokuwa na vyeti vya kuzaliwa lilifutwa na Rais John Magufuli kwa kuonekana kuwa litawaathiri mamilioni ya Watanzania wasiokuwa na vyeti hivyo.

Baadhi ya wachambuzi walidai kuwa Mwakyembe siyo waziri au kiongozi wa kwanza kutoa taarifa zilizomlazimu Rais Magufuli kuingilia kati kwa manufaa ya Watanzania na hivyo, wanapaswa kujua kuwa wana wajibu mkubwa kwa taifa na kutakiwa wajiepushe na matamko binafsi yasiyofanyiwa kazi kwa kina kabla ya kutolewa kwa umma.

“Ni vizuri kwa kila waziri au kiongozi yeyote yule kujipa uhakika wa kila tamko na amri wanazotaka kutoa kwa umma…kwa mfano, ni lazima wahakikishe kwamba wanazingatia sheria na pia wanayoyasema ni kwa maslahi ya umma mpana wa Tanzania.

“Vinginevyo, matamko yao yataendelea kuibua maswali na Rais hatakubali wamharibie kwa sababu ameshasema mara kadhaa kuwa daima atakuwa upande wenye maslahi kwa wananchi wake, na hasa wanyonge,” alisema mmoja wa wachambuzi hao.

“Ni vizuri wakaachana na matamko yenye viashiria vya kuwa na kiki za kuonyesha kuwa nao wako vizuri kuendana na kasi ya serikali ya sasa...wasipozingatia hayo kila mara watajikuta wakiwa tofauti,” mwingine aliongeza.

Neno ‘kiki’ ni la mtaani na limejitwalia umaarufu katika siku za hivi karibuni, likitumiwa kumaanisha mbinu zinazoweza kutumiwa na mtu ili kujipatia umaarufu juu ya jambo fulani. Wasanii na wanasiasa huhusishwa zaidi na neno hilo kutokana na asili ya kazi zao ambazo huwakutanisha zaidi na watu.

Awali, katika agizo lake hilo ambalo alilisisitiza pia jana asubuhi wakati akizungumza na kituo kimoja cha redio jijini Dar es Salaam, Mwakyembe alisema wameamua kuzuia ndoa kwa watu wasiokuwa na vyeti vya kuzaliwa kwa nia ya kuondokana na takwimu za sasa zinazoonyesha kuwa Tanzania Bara ni ya mwisho barani kwa utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa wananchi wake.

Alisema ni asilimia 12 tu ya Watanzania walioko Bara ndiyo wenye vyeti vya kuzaliwa na kuzidiwa hata na Zanzibar yenye wastani wa asilimia 75, hali aliyosema inashangaza kwa sababu bei ya vyeti hivyo ni Sh. 3,500 tu huku gharama za harusi zikiwa kubwa kulinganisha na kiasi hicho.

Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi kabla ya kuondoka mjini Dodoma na baadaye taarifa yake kusambazwa kwa umma jana, Rais Magufuli alisema anatengua uamuzi huo wa Waziri Mwakyembe kwa sababu utawanyima fursa ya kuoana Watanzania ambao wengi wao hawana vyeti hivyo vya kuzaliwa, hasa wale wa vijijini.

Alisema hadi sasa idadi ya Watanzania walio na vyeti vya kuzaliwa ni chini ya asilimia 20 huku wengi wao wakiwa ni wananchi waishio vijijini ambako ni vigumu kupata vyeti hivyo, na wengine wakiwa ni waliozaliwa kabla ya kuanza kutolewa kwa vyeti vya kuzaliwa nchini mwaka 1961.

“Kwa hiyo ndugu zangu Watanzania msiwe na wasiwasi wowote, endeleeni na utaratibu wenu wa kuoa na kuolewa kama kawaida na kama kuna kifungu chochote cha sheria kinachomlazimisha mtu awe na cheti cha kuzaliwa ndipo aoe ama aolewe nitamuelekeza Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Harrison Mwakyembe apeleke Bungeni kikarekebishwe” alisema Rais Magufuli, huku akitoa wito kwa wanasheria kuziangalia vizuri sheria zinazohusiana na kuzaliwa na kifo na kuoa na kuolewa ili zisilete mkanganyiko kwa wananchi.

JPM ALIVYOZIMA ‘KIKI’
Mbali na tukio la kuzimwa kwa ‘kiki’ ya Waziri Mwkayembe jana, wapo pia mawaziri na viongozi wengine kadhaa wa serikali na taasisi za umma waliokumbana na rungu la Magufuli la kutengua amri au tarifa zao. Hao ni pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama; Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.

Mhagama alikumbana na mkasa huo Machi 3, 2016 wakati alipotoa taarifa ya kumteua Dk. Carina Wangwe kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF). Hata hivyo, wakati uamuzi wake ukimpa umaarufu siku hiyo kupitia ‘kiki’ za kwenye mitandao ya kijamii, waziri huyo alilazimika kubatilisha taarifa hiyo kabla Rais Magufuli hajamtangaza Prof. Godius Kahyarara kushika nafasi hiyo NSSF.

Agosti 12 mwaka jana, Simbachwene alisisitiza kuondolewa kwa wamachinga maeneo ya mijini. Hata hivyo, siku chache baadaye, Magufuli alitengua agizo hilo wakati akihutubia jijini Mwanza kwa kutaka wamachinga wasiondolewe kwenye maeneo wanayofanyia biashara hadi pale mamlaka husika zitakapohakikisha kuwa zimewatafutia sehemu za kwenda kufanyia biashara zao.

Waziri mwingine aliyekumbwa na rungu la Magufuli hivi karibuni wakati kauli yake ikiwa imepamba moto na kuibua mijadala kwenye mitandao ya kijamii ni Nape.

Machi Mosi mwaka huu, Nape alielezea umuhimu wa kulinda majina ya wasanii waliotajwa hadharani wakituhumiwa kuhusika na dawa za kulevya, akisema kwamba ni vyema kuzingatia nguvu kubwa walizotumia kujijengea majina hayo na kwamba, ifikiriwe pia ni kwa namna gani watasafishwa ikiwa wataonekana baadaye kuwa hawahusiki na dawa za kulevya.

Nape alizungumza hayo akiwa Dodoma na baadaye kwenye kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na ITV kuelezea hatua iliyochukuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aliyetangaza hadharani majina ya wasanii kadhaa katika orodha yake ya awali ya watuhumiwa 65 wa dawa za kulevya.

Hata hivyo, siku chache baadaye, Magufuli alionekana kupinga maelezo ya Nape kwa kusisitiza kuwa vita dhidi ya dawa za kulevya isiangalie majina ya watu kwa sababu athari zake ni kubwa kwa taifa.

WALICHOSEMA WABUNGE, WASOMI WANENA
Akizungumzia suala la Mwakyembe, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema), alisema ni ishara kuwa baadhi ya mawaziri na viongozi wengine wamekuwa wakikurupuka kwa kutoa matamko bila kuyafanyia utafiti wa kina na ndiyo maana Magufuli ametengua agizo alilotoa kuhusu amri ya kuzuia ndoa kwa wasiokuwa na vyeti vya kuzaliwa.

Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni (CCM), alisema awali alikuwa haamini na mwishowe akajikuta akisikitika kusikia tamko la Waziri Mwakyembe kuhusu zuio la ndoa kwa wasiokuwa na vyeti vya kuzaliwa kwa sababu agizo lake halikuwa na msingi wa kisheria.

Alisema kupitia mkasa huo wa Mwakyembe, mawaziri wanatakiwa kuwa makini katika kutoa matamko ya aina hiyo na kwamba, kama wana hoja wanatakiwa kupeleka ndani ya Bunge ili ijadiliwe.

“Kama unatoa tamko leo na Rais analipinga ama kulifuta, hiyo inaonyesha kuwa waziri umekurupuka… matamko kama haya yanamgombanisha Rais na wananchi wake. Mawaziri wajiepusha kutoa matamko ambayo hayajapewa ridhaa,” alisema Chegeni.

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe, alisema alichokifanya Rais Magufuli kutengua tamko hilo yupo sahihi kwa kuwa suala la ndoa linagusa imani ya mtu na serikali haitakiwi kuingilia, na kwamba kama kuna jambo la kisheria liwasilishwe bungeni ili lifanyiwe kazi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Richard Mbunda, alisema inavyoonekana, huenda tangazo alilitoa Mwakyembe ni binafsi kwa mtazamo wake baada ya kuona kuna udanganyifu mkubwa katika eneo hilo.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Bindamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba alisema agizo la Mwakyembe kuhusu masuala ya ndoa linashangaza kwa sababu halipo kwa mujibu wa sheria

“Katika Sheria ya Ndoa, vitu ambavyo mtu anatakiwa kuwa navyo ili afunge ndoa ama sifa, hiyo ya cheti (cha kuzaliwa) haipo… sijui huyo Waziri ameitoa wapi na pia ingekuwepo kisheria ingepingwa kwa sababu watu wengi hawana vyeti vya kuzaliwa,” alisema Bisimba.


Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Ally Bashiru, alisema ni vyema Rais Magufuli ameingilia na kutengua agizo la Mwakyembe la kuzuia ndoa kwa asiokuwa na vyeti vya kuzaliwa

Hakuna maoni