Header Ads

PICHA:Picha:Rais Magufuli afanya ziara ya kushtukiza bandari ya Dar


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 23 Machi, 2017 amefanya ziara ya kushtukiza katika bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa kwa nyakati tofauti juu ya kudhibiti udanganyifu wa mizigo inayoingia na kutoka nchini kupitia bandari hiyo ikiwemo usafirishaji wa mchanga wa madini kwenda nje ya nchi.
Katika ziara hiyo Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia makontena 20 ya mchanga wenye madini kutoka kwenye migodi iliyopo kanda ya ziwa ambayo yamezuiliwa kusafirishwa nje ya nchi tangu alipotoa agizo la kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga nje ya nchi tarehe 02 Machi, 2017.
Pamoja na kushuhudia makontena hayo, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP – Ernest Mangu na vyombo vingine vya dola kuhakikisha mchanga wa madini unashikiliwa popote ulipo, mpaka hapo uchunguzi wa kina utakapofanyika kubaini ukweli.
“Nataka niwaambie nchi yetu inachezewa mno, nimekuja kuyaona haya makontena kama yapo, na kweli nimeyaona, sasa utaratibu utakapokamilika nataka Watanzania na dunia nzima ione kilichomo humu ndani kama ni mchanga kweli ama dhahabu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Akiwa bandarini hapo Mhe. Dkt. Magufuli pia ameshuhudia udanganyifu mwingine unaofanywa na wafanyabiashara wanaoagiza mizigo kutoka nje ya nchi baada ya kuoneshwa makontena ambayo nyaraka zinaonesha yamebeba mitumba ya nguo na viatu wakati ndani yake kila kontena moja limebeba magari matatu ya kifahari.
Maafisa wa bandari ya Dar es Salaam na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wamemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa kufuatia maelekezo aliyoyatoa ya kuhakikisha mizigo yote inakaguliwa kwa mitambo ya mionzi (Scanning Machines) wamefanikiwa kubaini udanganyifu mwingi unaofanywa na wafanyabiashara wanaoingiza nchini na kusafirisha nje ya nchi mizigo mbalimbali yakiwemo makontena 10 ambayo yamepatikana yakiwa na magari ya kifahari ilihali nyaraka zake zikionesha yana mitumba ya nguo na viatu.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza maafisa na wafanyakazi wa bandari ya Dar es Salaam na TRA kwa kazi nzuri wanayofanya kudhibiti upotevu wa fedha za umma bandarini hapo na amewataka kuendelea kutekeleza wajibu wao kwa uzalendo na kujiepusha na rushwa.
“Leo mmenifurahisha sana, ninawatia moyo endeleeni kuwakamata wote wanaofanya udanganyifu huu na muwachukulie hatua kali za kisheria, lakini msimuonee mtu na msipokee rushwa, tunataka watu wajifunze kuwa hapa sio shamba la bibi” amesisitiza Rais Magufuli.
Aidha, ametoa wito kwa vyombo vyote vinavyoshughulikia udhibiti wa mizigo inayoingia na kutoka kupitia bandari ya Dar es Salaam na bandari nyingine hapa nchini, kuendelea kushirikiana ili kukomesha vitendo vyote vya udanganyifu ambavyo vinasababisha nchi kupoteza mapato mengi.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam kufatilia maagizo yake ya kudhibiti vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na wafanyabiashara wanaogiza na kusafirisha vitu mbalimbali nje ya nchi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akihesabu makontena 20 yenye mchanga wa madini ambapo ameamuru kontena hizo zisisafirishwe mahali popote







Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza kuhusu makontena 20 yenye mchanga wa madini uliokuwa usafirishwe kwenda nje ya nchi ambapo ameagiza Kontena hizo zisisafirishwe mahali popote.

Makontena 20 yenye mchanga wa madini yakiwa yamezuiwa kusafirishwa nje ya nchi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli mara alipofanya ziara ya kushtukiza katika bandari ya Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akikagua nyaraka mbalimbali zenye kuhusu makontena ambayo husafirishwa nje ya nchi katika Bandari ya Dar es Salaam.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiangalia baadhi ya magari yalivyoingizwa nchini kwa njia isiyo halali ya kudai kuwa ni makontena ya mitumba wakati ndani yake wanaficha magari yakifahari pamoja na vitu vilivyochakaa March 23,2017


Moja ya kontena likiwa lina magari matatu ndani yake aina ya Range Rover ambapo muagizaji alidai kuwa anaagiza mitumba lakini kumbe ndani yake wanakuwa wameficha magari ya kifahari.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza jambo na IGP Ernest Mangu mara baada ya kufanya ukaguzi Bandarini hapo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

23 Machi, 2017

Hakuna maoni