MAKONDA: SITISHWI,NAULIZA WEWE NI NANI UNINYAMAZISHE NA UMETOKA WAPI?
MKUU
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ameadhimisha mwaka mmoja wa
kuwa kwenye kiti hicho kwa kula chakula cha mchana na waathirika wa dawa
za kulevya, huku akizungumzia mafanikio aliyopata katika uongozi wake.
Licha
ya kueleza mafanikio aliyopata, hakugusia kuhusu tuhuma mbalimbali
zilizoelekezwa kwake na watu mbalimbali, badala yake alisema hakuna wa
kumtisha wala kumnyamazisha na kwamba sasa ndiyo amepata nguvu mpya
baada ya kupata mashambulizi mbalimbali.
Pia
mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Maofisa wa Polisi, Oysterbay,
Dar es Salaam, ulihudhuriwa na watu wachache wakiwamo waandishi kutoka
vyombo vichache vya habari, tofauti na mikutano yake mingine ambayo
alikuwa akialika vyombo vingi vya habari.
“Mwaka
wangu wa pili katika uongozi ambao unaanza kesho (leo), speed (kasi) ya
hali ya utumishi wangu itaongezeka mara mbili zaidi kwa sababu
nimeshakomaa, lazima Dar es Salaam iwe kwenye mazingira salama.
“Eti
mtu anataka nikae kimya wakati wananchi wangu wa Dar es Salaam
wanateseka kwa matumizi ya dawa za kulevya… nauliza wewe ni nani
uninyamazishe na umetoka wapi?” alihoji Makonda.
Alisema
pamoja na changamoto nyingi anazopitia, hajawahi kutetereka wala
kutingishwa na kwamba yuko tayari idadi ya wanaomchukia iongezeke kwa
sababu hahitaji kupendwa.
“Sijawahi
kutetereka wala sijawahi kutingishwa. Kazi hii nimepewa na Mungu, acha
idadi ya wanaonichukia iongezeke kwa sababu sihitaji kupendwa, lakini
niwe na uhakika na Mungu wangu.
“Mara nyingi ninapochapwa na mawimbi makali, mke wangu amekuwa akizama kwenye sala na kuniombea,” alisema.
Alisema anafanya kazi hiyo kwa upendo na kwamba hana kisasi na yeyote.
“Tunayafanya
haya kwa upendo, hatuna kisasi na yeyote, ndiyo maana sisi tunafurahi,
lakini upande wa pili wanapambana, kazi yetu ni kumulika watu,” alisema
Makonda.
Aidha alisema wameamua kupigana vita ya dawa za kulevya hadharani kwa sababu hataki kupokea rushwa wala fedha haramu.
Makonda
alisema kupitia fedha za dawa za kulevya, wengi wamejenga maghorofa na
wamesababisha hata bei ya viwanja ipande, hivyo atahakikisha fedha hizo
zinakauka ili kila mtu ale kwa jasho lake.
Alisema
lengo lake ni kupambana kupigania ndoto za vijana na matumaini ya
wazazi wao na haijalishi kama amechelewa, lakini hataacha.
Makonda
alisema hababaishwi na watu wanaomchukia wakati akitekeleza majukumu
aliyopewa na Rais Dk. John Magufuli kama Mkuu wa Mkoa.
Alisema
wakiwaita wengine Kituo cha Polisi kwa vipimo, wamekuwa wakitumia dawa
ya meno aina ya Colgate na chumvi, lakini sasa wamekuja na mbinu mpya ya
vipimo.
“Wengine
tukiwaita kwa ajili ya vipimo, kwa wale ambao wanapimwa kwa njia ya
mdomo wanameza Colgate, wale wanaopimwa kwa njia ya mkojo wanaweka
chumvi.
“Mnakumbuka
wengine tulipowaita walikuwa wanachelewa kuja kumbe wanatumia vitu
hivyo ili wasigundulike, sasa tuna mbinu mpya za kuwapima,” alisema
Makonda.
MAFANIKIO YAKE
Akizungumzia mafanikio ya vita hiyo ya dawa za kulevya, Makonda alisema hadi sasa jumla ya waathirika 11,854 jijini Dar es Salaam wamekubali kuacha kwa hiari yao matumizi ya dawa hizo.
Alisema
hivi sasa wamepewa eneo kubwa la kujenga kambi kwa wahanga wa dawa za
kulevya, hivyo itawasaidia kufuatilia mienendo yao.
Makonda
alisema amefanikiwa kumaliza biashara ya shisha, ambayo ilikuwa
inatumiwa na baadhi ya wauzaji kuchochea matumizi ya dawa za kulevya.
Alisema
pia, kwa kushirikiana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, Kamishina Simon Sirro, wamefanikiwa kupunguza uhalifu wa aina
mbalimbali, ikiwamo ujambazi wa kutumia silaha na vikundi vya uhalifu
kama Panya Road.
MWAKA WA PILI
Makonda
alisema kuanzia wiki ijayo moto utawaka katika maduka ya kubadilishia
fedha (Bureau Change) kwa sababu zinatumika kuficha fedha haramu.
Alisema
katika Mkoa wa Dar es Salaam, fedha chafu zilikuwa katika maeneo mawili
ambayo ni bandari na dawa za kulevya, lakini sasa wamehamia katika
Bureau de Change.
“Dar
es Salaam hela chafu zilikuwa katika maeneo mawili; bandari na dawa za
kulevya, lakini hivi sasa maeneo hayo dili limekauka wamehamia kwenye
Bureau de Change… wiki ijayo moto utawaka, lazima tushughulike na
maficho haya,” alisema Makonda.
Alisema hivi sasa wataanza mfumo wa kutumia kadi ili wakusanye kodi na kila mtu ale kwa jasho lake.
Makonda alisema katika mwaka wake wa pili ataanza ziara katika Serikali za Mtaa aone jinsi watendaji wanavyowasaidia wananchi.
Akizungumzia
kuhusu wanaoishi mabondeni kama wana hati halali atawapatia viwanja,
lakini watendaji waliotoa hati hizo atawashughulikia.
“Nawaomba
wananchi wa Dar es Salaam wasikae maeneo hatarishi. Hatuwachukii bali
tunawapenda sana, hayo si maisha mazuri… najua wengi wanaoishi mabondeni
wamepangishwa na waliolipwa fidia, lakini huwezi kuwa na akili timamu
ukakubali kupanga bondeni,” alisema.
Alisema pia utakuwa ni mwaka wa kuhakikisha utendaji wa watumishi wa umma unaboreka na wananchi waache kuzungushwa.
Alitolea mfano ofisi ya ardhi aliyosema imekuwa ikizungusha watu pale wanapotaka kupata vibali vya ujenzi.
“Ukitaka
kibali watakusumbua, wakati mwingine watataka fedha ili waende kukagua
eneo lako, kisingizo ni kwamba hawana bajeti, lakini ukijenga bila
kibali watakuja kubomoa,” alisema Makonda.
Alisema kutoka na hali hiyo, asilimia 70 ya nyumba Dar es Salaam zimejengwa bila vibali.
Makonda
alisema pia mwaka wa pili katika uongozi wake utakuwa wa kushukuru,
hivyo kuwataka wananchi kujiwekea utaratibu wa kushukuru maofisa wa
Serikali wanaotimiza vyema wajibu wao.
Mipango
mingine aliyoieleza ni pamoja na kuelekeza maeneo ya kuuzia magari
(showroom), kuhakikisha Mahakama ya Ardhi ya Kinondoni inatenda haki na
kutoa hukumu kwa wakati na kwamba itafanya kazi hadi Jumamosi.
VITA DAWA ZA KULEVYA
Februari
2, mwaka huu, Makonda alitaja kwa mara ya kwanza majina ya baadhi ya
wasanii, akiwamo Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu na askari polisi
aliodai wanahusika na dawa za kulevya.
Siku
sita baadaye, alitaja majina mengine 65 ya watu maarufu akiwamo
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na
Uzima, Josephati Gwajima pamoja na mfanyabiashara maarufu, Yusuf Manji
akiwataka wafike Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam kuhojiwa juu
ya tuhuma hizo.
Februari
14, mwaka huu, Makonda alikabidhi majina mengine 97 ya watuhumiwa wa
dawa za kulevya kwa Kamishna wa Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers
Siyanga ambaye aliahidi kutoyatangaza hadharani kabla ya kuyafanyia
uchunguzi.
MAMBO AMBAYO HAJAYAGUSIA
Licha
ya kuwapo kwa shinikizo kutoka kwa makundi mbalimbali ya watu, wakitaka
Makonda ajibu tuhuma dhidi ya utata wa elimu yake na majina yake
halisi, jana hakugusia kabisa mambo hayo, badala yake alionekana
kuwajibu watu hao kwa mafumbo.
Hivi
karibuni, watu mbalimbali akiwamo Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima,
Josephat Gwajima, wameibuka na kueleza utata wa jina la mkuu huyo wa
mkoa pamoja na elimu yake.
Mara
kadhaa, Askofu Gwajima amekuwa akisema jina halisi la Makonda ni Daud
Albert Bashite na kwamba jina alilonalo sasa, alilipata baada ya kufeli
mitihani yake na kuchukua cheti cha mtu mwingine alichokitumia katika
masomo yake.
Mbali
na hoja hizo, baadhi ya wabunge katika mkutano wa Bunge uliopita,
walimtuhumu Makonda juu ya utajiri wake waliosema unatia shaka.
Baadhi ya mambo waliyosema ni umiliki wa magari ya kifahari na nyumba za kifahari zisizoendana na kipato chake.
Pia walisema moja ya kampuni binafsi imefanya matengenezo katika ofisi yake kwa mamilioni ya fedha.
Na ELIZABETH HOMBO-MTANZANIA DAR ES SALAAM
Post a Comment