HALI CHECHE:MADEREVA VIBURI WWONGEZEWA 'DOZI'
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Naibu Kamishna Mohamed Mpinga, aliyasema hayo mapema wiki hii, wakati akizindua mpango wa mafunzo ya usalama barabarani kwa walimu wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari 42 za jijini Dar es Salaam, ulioandaliwa na Taasisi ya Automobile Association of Tanzania (AAT).
Alisema kuanzishwa kwa mpango huo, kunatokana na baadhi ya madereva ambao si waadilifu ambao wamekuwa wakikiuka sheria za usalama barabarani wakati wa usiku na kusababisha ajali.
"Ingawa kwa sasa tuna changamoto ya upungufu wa askari wa usalama barabarani lakini tumejipanga kukabiliana na changamoto za usalama barabarani kwa kudhibiti madereva wazembe barabarani hasa wakati wa usiku kwa kuhakikisha tunafanya kazi kwa saa 24," alisema.
Kadhalika, alisema idadi ya ajali za barabarani zinazidi kupungua kila mwezi na kwamba jeshi hilo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanao toa elimu kuhusu usalama barabarani, watasaidia kuendelea kupunguza tatizo hilo kama si kumaliza kabisa.
Alisema katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Desemba mwaka jana, hadi Februari mwaka huu idadi ya ajali, vifo na majeruhi imepungua.
Kamanda Mpinga alisema, Desemba ajali zilikuwa 705, vifo 262 na majeruhi 598; Januari ajali zilikuwa 525, vifo 199 na majeruhi 459 na mwezi uliopita Februari ajali zilikuwa 453, vifo 198 na majeruhi 419.
"Kila mmoja akiwa balozi mzuri wa kuelimisha jamii kuhusiana na usalama barabarani tutamaliza tatizo hili. Naamini pia mafunzo haya muhimu ambayo walimu zaidi 1,000 watanufaika nayo, yatawafikia watu wengi zaidi kwa sababu nao wataelimisha wanafunzi na jamii kwa ujumla," alisema.
Naye Rais wa AAT, Nizar Jivani, alisema mafunzo hayo ya elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi wa shule za msingi, itakiwa chachu kwa kizazi kipya na cha baadae kwa ajili ya kupunguza ajali za barabarani kama ilivyo azimio la Umoja wa Mataifa.
Aidha, alimshauri Kamanda Mpinga kuwapo na mpango maalum wa kuzipa namba bodaboda na bajaji zote na utambulisho wa rangi kwa kila wilaya kama zilivyo teksi ili kuzibaini kwa urahisi zile zinazokiuka sheria na ziweze kuchukuliwa hatua kwa urahisi.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa AAT, Yusuf Ghor, alisema jumla ya vyuo na shule na vyuo vitakavyopata mradi huo ni 42 na viwili vikiwa ni vyuo vya ualimu, shule ya awali moja, shule za msingi 27 na Sekondari 12.
Alisema wanatarajia walimu watafundisha mtaala wa mafunzo ya usalama barabarani na kwamba pia watawapatia vifaa vya kufundishia na vya kutumia kwa ajili ya wanafunzi kuvukia barabara
Post a Comment