Askari wawili wakamatwa kwa wizi wa mafuta ya ndege za ATCL
Kamanda wa Polisi kanda ya Dar es salaam Kamishna Simon Sirro, akizungumza, alisema kuwa uchunguzi wa kina umefanyika baada ya tukio hilo ili kubaini mtandao huo ambao unawahusisha askari wenye namba F.8419 CPL Bahati Msilimi na F.9901 PC Benaus Mkama.
Kamishna Sirro alisema, Machi 17, mwaka huu usiku kwenye hanga la kampuni ya shirika la ndege ATCL, Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, polisi wakishirikiana na maofisa usalama wa uwanjani hapo walimkamata Nyangasa akiwa na mafuta hayo ya ndege.
Aliongeza kuwa kuwa mafuta hayo yaliibiwa kutoka kwenye ndege ya 5H-MWF aina ya DASH 8-Q 300 mali ya kampuni ya ATCL iliyokuwa katika matengenezo kwenye hanga hilo.
“Baada ya uchunguzi wa kina wa wahandisi wa ATCL, ilibainika kuwa jumla ya lita 220 ndizo zilizoibiwa kutoka katika ndege hiyo na askari hao wameshakamatwa kwa uchunguzi zaidi na mara utakapokamilika watatuhumiwa na watafikishwa kwenye vyombo vya sheria”Alisema.
Kamishna Sirro alisema wizi wa mafuta ya ndege ni hatari kwa kuwa unaweza kuchangia kutokea kwa moto au ajali kutokana na kukosa mafuta.
Alisema imebainika kuwa mafuta hayo yamekuwa yakiuzwa kama mafuta ya taa.
Aidha alitoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo mengine nchini kuwa wasijihusishe na ununuzi wa mafuta ya aina hiyo na kama wakikamatwa watachukuliwa hatua kama washiriki wa makosa hayo.
Post a Comment