Header Ads

Tanzia: GOLIKIPA WA KAGERA SUGAR DAVID BURUHANI AFARIKI DUNIA

Golikipa wa timu ya Kagera Sugar, David Abdalah Burhan ambaye pia amewahi kuchezea klabu mbalimbali za ligi kuu amefariki dunia usiku wa kuamkia Jumapili katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza.
Kwa mujibu wa kocha wa timu ya Kagera Sugar Meck Mexime, Burhani ameugua tumbo siku tatu zilizopita walipofika Kagera alilazwa kwenye hospitali ya Kiwandani na kuwa baadaye macho yake yalianza kubadilika na kuwa ya njano.
''Tulifanya booking ya ndege kuelekea Bugando, tulichelewa, tukapata jana amefikishwa Bugando leo asubuhi tumepata taarifa kuwa amefariki dunia'' anafahamisha Kocha Mexime.
Hata hivyo anasema kutokana msiba huo watajaribu kuomba shirikisho la soka liahirishe mechi zake za karibuni hadi hapo watakapomaliza mazishi ya mchezaji mwenzao.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amethibitisha kutokea kifi hicho na kutuma salamu zake za pole kwa familia pamoja na klabu ya Kagera Sugar na kwa wote ambao wameguswa na kifo cha mchezaji huyo.
“Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha David Abdalah Burhan mchezaji wa Kagera Sugar. Amefariki usiku wa kuamkia leo.Apumzike kwa amani,” alitweet kiongozi huyo wa TFF.
Chini ya golikipa David Burhan timu hiyo ilifanikiwa kufanya vyema katika ligi hiyo mwaka 2013-14 kiasi cha kushika nafasi ya nne katika ligi hiyo.
Burhani aliondoka katika timu ya Mbeya City na kujiunga na timu ya Kagera Suger hadi kifo kilipomchukua.
Taarifa za kifo cha David Buruhani ambaye licha ya kufariki akiwa mchezaji wa Kagera Sugar, amewahi kuzichezea timu za Mbeya City na Majimaji, zinakuja ikiwa ni siku 57 zimepita toka Tanzania impoteze mchezaji Ismail Khalfan aliyefia uwanjani wakati wa mchezo dhidi ya Mwadui FC December 4 2016.

Hakuna maoni